WATUMISHI WA AFYA PWANI WAJENGEWA UWEZO KUKABILIANA NA MAGONJWA YA MILIPUKO

 


Na WAF, Pwani 

Wizara ya Afya, kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI, CDC Tanzania na Amref Health Africa Tanzania kupitia Mradi wa Global Health Security Agenda (GHSA), imeendelea kuwajengea uwezo watumishi wa afya katika halmashauri zote tisa za Mkoa wa Pwani, kwa lengo la kuimarisha utayari na uwezo wa kukabiliana na magonjwa ya milipuko, ikiwemo Ebola.

Mwakilishi wa Wizara ya Afya kutoka Kitengo cha Uhakiki wa Ubora wa Huduma za Afya, Dkt. Yohana Msigwa, amesema mafunzo hayo yanaambatana na tathmini ya utayari wa vituo vya kutolea huduma za afya, ambapo wataalamu wanakagua uwepo wa vifaa kinga, dawa za usafi, pamoja na uwezo wa watumishi kutumia vifaa hivyo kwa usahihi.

Dkt. Msigwa amesema hayo leo, Septemba 7, 2026, mkoani Pwani, wakati wa zoezi hilo linaloendelea katika halmashauri zote tisa za mkoa huo, akieleza kuwa tathmini hiyo inalenga kubaini uwezo wa vituo vya afya kukabiliana na magonjwa ya mlipuko na kuchukua hatua stahiki kwa wakati.

“Zoezi hili linahusisha tathmini ya vituo kama vinaweza kukabiliana na ugonjwa wa mlipuko. Tunaangalia uwepo wa vifaa kinga na dawa za kufanyia usafi, pamoja na kufanya mazoezi ya vitendo kwa watumishi ili kujikumbusha matumizi sahihi ya vifaa hivyo,” amesema Dkt. Msigwa.

Kwa upande wake, Msimamizi wa Ubora wa Huduma za Afya Mkoa wa Pwani, Denis Kapinga, amesema mafunzo hayo yanahusisha watumishi 25 wa afya kutoka kila halmashauri, pamoja na wataalamu wa tiba asili, ambao wamepewa ujuzi wa kutambua dalili zinazoweza kuashiria magonjwa ya milipuko na kutoa taarifa kwa mamlaka husika ili hatua zichukuliwe kwa wakati.

“Kama tunavyofahamu, katika huduma hizi kuna watu wanaamini katika tiba asili. Hivyo, tumewapa mafunzo wataalamu wa tiba asili ili waweze kutusaidia kuibua washukiwa wa magonjwa ya milipuko kama Ebola pindi wanapomwona mtu mwenye dalili, kwa kutupa taarifa ili tuweze kuchukua hatua kwa haraka,” amesema Kapinga.

Kapinga amesema kila halmashauri imeweza kutenga kituo kimoja cha matibabu kwa ajili ya kutoa huduma endapo kutatokea mgonjwa anayehitaji huduma maalum kutokana na ugonjwa wa mlipuko, hatua inayolenga kuimarisha utayari wa mfumo wa afya, kuwezesha hatua za haraka na kudhibiti kuenea kwa magonjwa hayo.

No comments

Powered by Blogger.